Neno Fupi La Usiku Huu: Mauaji Ya Usa River Na Kisa Cha Mtego Wa Panya
Ndugu zangu,
Kuna kisa cha mtego wa panya uliosababisha madhara hata kwa wasio panya.
Panya kwenye nyumba aliubaini mtego wa panya uliowekwa uvunguni mwa kitanda na mwenye nyumba.
Panya yule akamwendea jogoo wa mwenye nyumba. Akamwambia; " Ewe jogoo, kuna mtego umewekwa uvunguni mwa kitanda. Tusaidiane namna ya kuutegua kabla haujatudhuru wote".
Jogoo akajibu; " Ondoka zako, mie mtego wa panya unanihusu nini wakati sina kawaida ya kufika uvunguni mwa kitanda!"
Panya yule akaenda hadi kwa mbuzi wa mwenye nyumba. Akamwambia; " Ewe mbuzi mwema, unajua kuna mtego wa panya uvunguni mwa kitanda cha mwenye nyumba. Tusaidiane mawazo ya kuutegua kabla haujatudhuru sote".
Mbuzi akajibu; " Hivi tangu lini ukaniona nikiingia chumbani kwa mwenye nyumba? Mtego huo wa panya haunihusu mie mbuzi".
Panya akaenda hadi kwa ng'ombe wa mwenye nyumba. Akamwambia; " Ewe ng'ombe wa bwana, kuna mtego wa panya umewekwa uvunguni mwa kitanda. Tusaidiane mawazo namna ya kuutegua kabla haujatuletea madhara"
Ngombe akajibu akionyesha mshangao;
" Sijapata kusikia jambo la ajabu kama hilo. Yaani, mie ng'ombe nidhurike na mtego wa panya ulio uvunguni mwa kitanda! Hilo halinihusu."
Basi, ikatokea siku moja, nyoka akaingia chumbani kwa mwenye nyumba. Katika kutambaa kwake uvunguni mwa kitanda, mkia wa nyoka ukanasa mtegoni. Kishindo kilisikika.
Mwenye nyumba alikwenda kwa furaha akiamini hatimaye panya aliyekuwa akimsumbua sasa amenaswa. Hapana, ni nyoka aliyenaswa mkia. Na ni mwenye hasira pia. Akamng'ata mguu mwenye nyumba. Sumu kali akamwachia. Mwenye nyumba akafa.
Jirani wakafika msibani. Siku ya kwanza watu walikuwa wachache. Wakahitaji kitoweo . Akakamatwa jogoo wa mwenye nyumba achinjwe.
Siku ya pili watu wakaongezeka. Kilihitajika kitoweo pia. Akakamatwa mbuzi wa mwenye nyumba ili achinjwe.
Na siku ya maziko watu wakawa wengi zaidi. Akakamatwa ng'ombe wa mwenye nyumba ili achinjwe.
Ni jogoo, mbuzi na ng'ombe wa mwenye nyumba walioamini kuwa madhara ya mtego ule wa panya yasingewahusu wao. Walikosea. Panya alikuwa sahihi, na wala mtego haukumdhuru panya!
Naam, Watanzania tunazidi kupokea habari mbaya za matukio ya mauaji ya kutisha. Vuguvugu la mapambano ya kisiasa linasemwa kuwa ni moja ya sababu za matukio ya mauaji na hata watu kujeruhiwa kwa mapanga.
Na vuguvugu la mapambano ya kisiasa halipawi kuandamama na vitendo vya mauaji au kujeruhiana kwa mapanga, bali, liwe ni vuguvugu la mapambano ya hoja.
Kule Nyamagana tumeshuhudia wabunge wamepigwa mapanga. Na jana kiongozi wa Chadema pale Usa River amechinjwa kama kuku.
Inasikitisha sana kuona vitendo hivi vya kinyama vinazidi kuongezeka. Inasikitisha pia kuwa polisi wanashindwa kwa haraka kuwatia nguvuni wahusika wa mauaji na kuwafikisha mahakamani. Labda idara za upelelezi wa kipolisi zinahitaji kuimarishwa zaidi.
Na huu ni wakati, kwa Watanzania, bila kujali tofauti zetu za kiitikadi, kidini au rangi, tukemee kwa sauti moja vitendo hivi viovu. Kamwe tusikubali ikawa ni vitu vya kawaida.
Ni wakati sasa kwa wananchi wakiongozwa na viongozi waandamizi wa vyama vya siasa. Viongozi wa kidini na wanaharakati wa haki za kibinadamu, kusimama kwa pamoja, na kwa kauli na vitendo, kulaaani maovu haya na mengineyo yenye hata kupelekea roho za wanadamu wenzetu kutoweka.
Hakika, kama mtego ule wa panya, tutafanya makosa makubwa kama kuna watakaodhani, kuwa haya ya watu kuchinjwa na kujeruhiwa na mapanga yatawakuta watu wa kundi fulani tu. Tukiacha yaendelee, basi, yeyote yule, bila kujali dini, rangi, itikadi au hata wadhifa wake, anaweza kuwa mhanga wa maovu haya. Kama taifa, kwa pamoja tuwalaani wauaji hawa.
Na hilo ni Neno Fupi la Usiku Huu.
Maggid Mjengwa,
Iringa.
Habari kwa hisani ya mjengwa blog