WHATEVER YOUR ARE BE A GOOD ONE;

A nation that is afraid to let its people judge the truth and falsehood in an open market is a nation that is afraid of its people. John F. Kennedy

“Taifa letu – taifa lolote – ni zuri na mahali pazuri pa kuishi kama raia wake watalifanya liwe hivyo. Uongozi wake unaweza kuwa mzuri, mbaya au usiojali lakini kama watu wake wameamka (ki-elimu?) na wanajitambua, haitachukua muda mrefu kuwakilisha mtazamo wa jamii na kubadili mawazo na matumaini ya taifa.” Julius Kambarage Nyerere


Tuesday, February 21, 2012

MUGABE NA DEMOKRASIA



Akitimiza miaka 88 leo Rais wa Zimbabwe Robert Mugabe aliyetawala toka uhuru wa nchi nchi hiyo1980,  leo amesema bado ataendelea kugombea uraisi wa nchi hiyo mpaka pale atakaposema mwenyewe imetosha..
Habari kwa Hisani ya Mjengwa Blog



Monday, February 20, 2012

LEADERSHIP CORNER

Most people spend more time and energy going around problems than in trying to solve them. - Henry Ford

Sunday, February 19, 2012

Uchambuzi Wa Habari: Dk Mwakyembe Naye Amwaga Sumu!



Ndugu zangu,

Kwenye vyombo vya habari kumekuwa na taarifa zinazochanganya  juu ya kinachomsibu Dk. Mwakyembe.

Na kama utangulizi ufuatao nitauzungumza kama hotuba fupi mbele ya watu wanaojiandaa kwa mlo wa kusheherekea harusi, basi, nina imani, zaidi ya nusu ya wageni waalikwa watainuka kwenye meza zao na kukiacha chakula.

Maana nitaanza kwa kusema;

Mabibi na Mabwana,

Wakati tukijiandaa kwa  mlo ulio mbele yenu ningependa kuwaeleza mafupi juu ya sumu na jinsi sumu inavyoweza kuingia kwenye mwili wako na hatimaye kukudhuru. Na bila shaka wote mnajua kuwa sumu inaua.

Ni hivi; unaweza kuwekewa sumu. Usipoiona na ukaiacha, basi, utakuwa umepona.  Ndio, kama kuna sumu imewekwa usiichukue. Kwa mantiki hiyo hiyo, jiadhari, unaweza ukashikishwa sumu.  Kuwa makini na wanaokupa mikono ya heri, mingine ni mikono ya kifo. Yumkini anayekupa  mkono amevaa glovu yenye sumu.

Ndugu yangu, unaweza pia   ukagusishwa sumu.  Kuwa makini na unayecheza nae muziki baada ya mlo huu. Kumbatio la muziki tulivu laweza kugeuka kuwa ni kumbatio la kifo.

Sumu inaweza  pia kukuingia  mwilini kwa kulishwa.  Uwe makini na anayekulisha kipande cha keki ya harusi. Na kama waweza kulishwa sumu hivyo hivyo waweza ’ kujilisha’ mwenyewe sumu. Chunga sana na anayekupa kipande cha nyama choma. Ukakipokea na hatimaye kukitia mdomoni.

Kama ilivyo kwa kulishwa na kujilisha sumu. Yawezekana pia sumu ikaingia mwilini mwako kwa kunyweshwa au kujinywisha.  Chunga sana na unayekaa karibu naye. Jichunge mwenyewe pia. Ukinywa vodka nyingi ni sawa na ’ kujinywisha’ mwenyewe sumu.

Sumu yaweza pia kukuingia mwilini kwa kumwagiwa. Kaa mbali sana na atakayefungua champeini isije kilichomo kikawa ni sumu.  Na wengine hamfahamu, kuwa   sumu yaweza  pia kukuingia kwa kupuliziwa.  Sahani yako ya chakula yaweza kuwa imepuliziwa sumu…

Ndugu zangu,

kuna njia nyingi sana za sumu kuingia mwilini mwako. Nisiwachoshe, tuendelee na  mlo wetu wa harusi!

Naam. Habari kubwa katika siku mbili hizi ni kadhia ya Dr. Mwakyembe na madai ya  sumu kuingizwa mwilini mwake na wabaya wake. Na kama mlivyoona hapo juu, bado haijawa wazi kama Mwakyembe kalishwa, kawekewa, kanyweshwa au kagusishwa sumu. 
Jitihada za Jeshi la Polisi juzi kutaka kutuambia WaTanzania ukweli juu ya kadhia hii zinaonekana kugonga mwamba  kwa kupingwa vikali na Mwakyembe mwenyewe. Tumesoma kwenye magazeti ya leo.

Nani anaongopa?

Bila shaka, habari hii imekuwa ikiwavutia wengi kwa vile kiu ya jamii ni kutaka kujua ukweli mzima. Jamii inataka kujua; nani anasema kweli na nani anaongopa. Vita inayopiganwa sasa imebaki kuwa ni vita ya maneno kwenye vyombo vya habari.

Kila upande unadai una ushahidi na unachosema lakini ushahidi huo hauwekwi hadharani ukaonekana.  Wanahabari nao wameonekana kusukumwa zaidi na upepo wa vita na kuandika yale ambayo wanadhani yatauza magazeti.  Kimsingi media inaweza ikamaliza vita hii kwa kuwauliza wahusika maswali sahihi na magumu yatakayotokana na  maelezo wanayotoa wahusika

Mfano, DCI Manumba anasema; ” Ukweli kuhusu  kauli hiyo inayodai kuwekewa sumu , tumeupata baada ya kuwasiliana na Wizara ya Afya ambayo nayo imewasiliana na  hospitali aliyokuwa amelazwa  Dk Mwakyembe nchini India. Taarifa zinaonyesha  kuwa hakuna sumu  katika maradhi yanayomsibu Mwakyembe.”- ( Mwananchi, Jumamosi, Februari 18, 2012)

Naam, kama DCI Manumba anadai wamethibitishiwa na Wizara ya Afya iliyofanya mawasiliano na hospitali anayotibiwa Dr . Mwayembe nchini India  kwamba Dr Mwakyembe hakukutwa na sumu mwilini ni kwanini wanahabari wasifike Wizara ya Afya kuthibitishiwa juu ya kile ambacho Manumba anadai kuthibitishiwa. Maana, haiyumkini kuthibitishiwa huku kukawa ni kwa mdomo tu.
Na Dk. Mwakyembe anaposema; ” Ripoti inatamka wazi kuwa  kuna kitu kwenye bone marrow ( ndani ya ute wa mifupa) kinachochochea hali niliyonayo, kitu ambacho mabingwa wanahangaikia kukijua.” ( Mwananchi,  Februari 19, 2012.)

Kwa wanahabari kazi hapa ingekuwa kumbana Mwakyembe  awasaidie kupata maelezo ya ziada kutoka kwa mabingwa hao wa India ili iwasaidie ku-establish, bila mashaka, juu ya dhana ya sumu katika kinachomsibu Mwakyembe.

Vinginevyo, taarifa ya jana ya Dr Mwakyembe inatoa tafsiri pia ya mtu aliyejeruhiwa na aliyeamua ’kumwaga sumu’ hadharani. Taarifa ile ya Mwakyembe imeonyesha jinsi  watendaji wetu wakuu Serikalini na hata kwenye chama tawala wasivyoaminiana. 

Tumeona jinsi Mwakyembe alivyorusha makombora makali dhidi ya jeshi la polisi na kutoa tuhuma nzito ya jinsi  jeshi hilo linavyotenda hujuma . Kwa mtu wa kawaida atajiuliza; kama Mwakyembe Waziri na kada wa CCM analia kuchezewa faulo, je,  hali itakuwaje kwa mtu wa kawaida na kama ni mwanachama wa chama cha upinzani?

Swali lingine; kama baadhi ya mawaziri wa JK kwenye baraza moja wanaonyesha hadharani kuwa hawaaminiani wanamsaidiaje Rais wa nchi? Na je, Mwakyembe au Sitta wakihamishimiwa wizara ya Mambo ya Ndani  watafanyaje kazi na akina Manumba na Said Mwema? Na kuna wengi wanaomtarajia JK kufanya  mabadiliko makubwa  ya Baraza la Mawaziri kwa vile hawaridhishwi na utendaji wa Baraza lililopo.

Na haya yote tunayoyashuhudia  ni ’ maradhi ya taifa’  ya tangu uhuru kwa vile tumekuwa na Katiba yenye mapungufu makubwa na kwa sasa isiyokidhi mahitaji ya wakati uliopo. Tunamshukuru Rais wa nchi kwa kuonyesha dhamira ya kutuanzishia mchakato utakaopelekea kupata Katiba Mpya kwa Taifa la Kisasa.

Katiba ya sasa inaruhusu ’ ubaguzi wa kisiasa’. Inawatenga Watanzania wengine katika ushiriki wa uongozi na ujenzi wa nchi.  Na dhambi ya ubaguzi ndio inayotutafuna sasa hadi tukafikia hata viongozi watendaji wa juu ndani ya chama tawala  kukosa kuaminiana.
Ndio, Watanzania walio wengi  ’ hawajalishwa sumu’, isipokuwa, kwa miaka mingi Watanzania wamekuwa ’ wakibwigizwa ugoro’ uliowafanya wasinzie  kama watu waliopigwa  sindano ya ganzi.

Wengi  sasa , na hususan vijana, wanakataa mchana wa jua kali kubwigizwa ugoro na walio kwenye mamlaka. Wamebumbuluka. Wameanza kusoma katikati ya mistari. Ndio, wameamka na wana kiu ya kuiona Tanzania mpya na inayostawi. 

Maggid Mjengwa,
Dar es Salaam.
Jumapili, Februari 19, 2012.

Habari kwa hisani ya Mjengwa Blog

Thursday, February 16, 2012

WHAT IS LEADERSHIP?


Leadership is understanding people and involving them to help you do a job. That takes all of the good characteristics, like integrity, dedication of purpose, selflessness, knowledge, skill, implacability, as well as determination not to accept failure. - 

Admiral Arleigh A. Burke

Thursday, February 9, 2012

THIS IS GREAT


A friend is someone who knows the song in your heart and can sing it back to you when you have forgotten the words. - Unknown

MIGOMO NA KUKOSEKANA KWA EFFECTIVE COMMUNICATIONS




KWA NINI SWALA LA MIGOMO LINACHUKUA MUDA MREFU KUPATA UFUMBUZI?

Kama wataalamu wengi walivyowahi kusema huku nyuma kuwa chanzo cha migomo mingi kutokea na kuchukua sura mpya inatokana na  kupungua kwa mawasiliano miongoni mwa  pande mbili ambazo zinatofautiana au kama kuna mawasiliano mawasiliano hayo yanakuwa hayakubaliki kwa upande mmoja au kutohusishwa moja kwa moja katika majadiliano husika katika  kututua tatizo husika. 




Tatizo wakati mwingine wakati wa majadiliano mhusika mkuu mara nyingi Serikali  anachokizungumza pengine kinatia mashaka ya ukweli wa suluhu;  Baba Wa Taifa akikuwa akisuluhisha Mgomo  wengi walikuwa wakijenga imani  kwani  alichokuwa akikiongea unaona kabisa anachosema ndio anachomaanisha. Tofauti na viongozi wetu wa sasa mara nyingi wanachoongea na hali halisi ni tofauti kwani wanachukua mno hali ya kujilinda zaidi  na mbaya zaidi wanakimbilia kutupa taarifa ambazo zinaongeza wasiwasi baada ya kutatua tatizo.




Nafikiri katika hali yeyote ile serikali kama msimamizi wa sera na  taratibu za maisha ya watanzania katika hali ya migomo  ambayo imeendelea kujitokeza katika taifa letu, tunahitaji uthubutu katika kutatua tatizo hili;

Katika sakata la mgomo wa serikali na  madaktari ambao umedumu kwa takribani wiki tatu sasa;

  • Swali ambalo tunahitaji kujuuliza leo ni hili  Hivi serikali imeonyesha nia ya kumaliza mgogoro huo katika meza ya majadiliano mapema?

  • Je madaktari  wanajisikia vipi wakiona ndugu zao marafiki au watanzania wakipoteza maisha kwa kukosa hudumu muhimu ya afya ikiwa ni  sehemu haki ya wananchi kikatiba?

  • Nafikiri Majadiliano na maelewano ni sehemu muhimu katika kufikia muafaka wa migogoro



Hii ni vita ya mafahari wawili na wanaoumia kwa kiasi kukubwa ni wananchi ambao hawana kosa pamoja na mchango mkubwa mkubwa wa kodi zao wameishaia kupoteza maisha na kwa mvutano unaoendelea;



Ni kweli kuwa Ikumbukwe kuwa, serikali ikitenda wajibu wake na  na kutoa haki kwa wahusiaka bila upendeleo  kwa wakati  sahihi kwa kila jamii ambayo inahusika kulingana na tatizo linalosababisha mgomo. Migomo mingi ambayo inajitokeza katika taifa letu inahusiana na tatizo la uwiano wa masilahi (mishahara) katika jamii pale panapotokea  tofauti ya mishahara iliyowekwa kwa makusudi ya kuwapa nafuu wafanyakazi wa kundi moja ndiyo inayotumiwa katika kudai nafuu ya wajibu na haki kwa kundi lingine.

Pengine hata swala la mgomo huu wa madaktari katika kipindi hiki unaweza kusababisha na mvutano wa posha za viongozi wetu watunga sheria (wabunge) ambao walitaka walipwe posho ya shilling 200,000 kutoka elfu sabini;(70,000) hii ni assumption moja ambayo imekuwa kichocheo cha mgomo;

Kama ni kweli kwa nini  wanasiasa  wanajifikira sana wao wenyewe na kujijengea hoja na kubeza hoja za wananchi  au makundi mengine ndani ya jamii hasa wanapozungumzia masilahi;  ni ukweli ambao haufichi kuwa wanasiasa ambao ni watawala amabo tumewapa dhamana ya kutuongoza  mara nyingi wanajitengenezea masilahi bora, posho  nono na marupurupu mengine yanayowafanya waishi maisha bora na pale wanapoumwa na familia zao wanatibiwa nje ya nchi. 


Mwalimu Nyererealiwahi sema kuwa , “leo ukigoma unamgomea nani; tafakari matokeo!”  Jibu ni rahisi kada zinagoma kwa kukosa majibu sahihi ya maswali yao, na kukosekana kwa effective communication ya madaia husika.

Mwalimu Nyerere kwenye alitukumbusha kuwa , “Wafanyakazi wa Tanzania wanayo haki ya kuheshimiwa na wafanyakazi wengine na wananchi wote. Lakini kwa heshima yao wanayoipata, lazima wafanyakazi wote wakubali kufanya kazi kwa bidii. Ndiyo kusema kwamba kila mfanyakazi lazima afuate masharti ya kazi anayopewa. Kama kwa sababu fulani hayapendi masharti hayo, anaweza kupeleka shauri hilo katika kikao kwa utaratibu uliokubaliwa. Lakini kwa sasa lazima atafuata masharti yaliyopo.”

Tatizo la wakati wetu tabaka la masilahi bora linaongezeka na kusababisha  migomo  miongoni mwa jamii; kwa viongozi wetu na wanansiasa wetu nafikiri ni wakati mwafaka wa kuitafakari hali hii na kuijengea mikakati ya kuhakikisha kuwa migomo inatokomea kabisa ndani ya jamii zetu; Hakuna lisikowezekana; Pamoja tukisima tutaendelea kwa faida ya wote

Monday, February 6, 2012

NEW CONSTITUTION PROCESS IN TANZANIA


We must become the change we want to see.
 By : Mahatma Gandhi

Uchambuzi Wa Habari: Alichosema Ali Mufuruki



Ndugu zangu,

Kwenye gazeti la Mwananchi jana Jumapili kulikuwa  na habari ukurasa wa tano inayosema; “Mufuruki: Itikadi za kisiaa zinakwamisha wananchi”.  ( Mwananchi Jumapili, Februari 5, 2012)

Habari hiyo ilinivutia sana na ikawa ya kwanza kwangu kuisoma. Mwandishi Exuper Kachenje anaripoti, kuwa  Mwenyekiti wa Jukwaa la Maafisa Watendaji Wakuu wa Kampuni Binafsi nchini  Bw. Ali Mafuruki ametaja kuwa itikadi za kisiasa ni  vikwazo vikubwa  vilivyowanyima  na vinavyoendelea kuwanyima  wafanyabiashara wazalendo nafasi  wakiachwa nyuma  na kuwapendelea  wageni wanaoshikilia uchumi wa Tanzania kwa kiasi kikubwa.

Ali Mufuruki anasema; ” Vikwazo vikubwa kuliko vyote ambavyo mpaka leo vipo ni vile vilivyotokana na itikadi ya kisiasa ambavyo siyo tu ilimnyima nafasi mfanyabiashara mzalendo, bali pia iliwapendelea zaidi wasio wazalendo.”- Ali Mufuruki.

Mufuruki anazidi kubainisha, kuwa kwa muda mrefu Watanzania wengi wenye uwezo wa kufanya biashara kubwa walikimbilia kufanya kazi za kuajiriwa Serikalini, kwenye shughuli za za siasa huku wasio na uwezo  wa kupata ajira  wakihangaika na biashara ndogondogo na kuiacha sekta ya biashara kubwa kwenye mikono ya watu wenye asili ya kiasia.

Bwana Mufuruki akazidi kuwa mkweli na kusema, kuwa waasisi wa Uhuru wetu  walitilia mkazo zaidi udhibiti wa nguvu ya utawala wa kisiasa bila kujali nafasi ya wananchi wao katika kudhibiti nguvu za uchumi. Hilo, kwa mujibu wa Mufuruki, ndilo  lililowaacha  wenye uwezo zaidi kudhibiti nguvu za uchumi wa nchi kwa miaka mingi ijayo.

Mtazamo wangu;

Bwana  Ali Mufuruki amekuja na hoja  ya kizalendo, nzito na muhimu sana kwa nchi yetu kwa sasa. Watanzania tumekuwa kama wagonjwa wa muda mrefu ambao,  waganga mbali mbali  tuliowapata wameshindwa kutwambia chanzo cha maradhi yetu. Hivyo basi, wameishia kujaribisha tiba , moja baada ya nyingine, bila mafanikio. Watanzania bado ni  wagonjwa kiuchumi.

Ali Mufuruki ametusaidia kujua chanzo cha maradhi yetu. Na yuko sahihi kabisa. Alichokisema Mufuruki mara kadhaa nimekiita kuwa ni ubaguzi wa kisiasa. Nchi yetu inasumbuliwa na ’maradhi ya ubaguzi wa kisiasa’. CCM , kama ilivyokuwa kwa TANU, bado inaamini katika udhibiti wa nguvu za kisiasa.

Kuna mifano kadhaa  ya Watanzania wazalendo waliofilisika kibiashara kwa ’ dhambi ya kuwaunga mkono wapinzani’. Tuna mifano kadhaa ya wafanyabiashara Watanzania wenye asili ya kiasia ambao biashara zao zinashamiri kwa vile walichagua tangu enzi, kuwa wafadhili wa TANU na baadae CCM ambayo ina hamu ya kuendelea kudhibiti nguvu za kisiasa badala ya kuandaa mazingira ya wananchi wake wadhibiti uchumi wao.

Wakati CCM ikitimiza miaka 35, hoja ya Ali Mufuruki waichukulie kama changamoto.  Maana, zama za udhibiti wa nguvu za  kisiasa zimepita.  Kwenye pluralism kuna ustawi . Kwenye  ' Chama Kushika Hatamu' kuna kudumaa. Huwezi leo kuendelea na udhibiti wa nguvu za kisiasa kama wananchi wako hawana udhibiti wa nguvu za kiuchumi na badala yake udhibiti huo huko mikononi mwa wananchi wako wachache wenye asili ya kiasia au wageni wanaoitwa wawekezaji.

Na huu si wakati tena wa kuwa na wanasiasa wenye kutoa hadharani, kauli kama; ” Anayetaka biashara yake imwendeee vizuri aje CCM!”

Tubadilike ili tusonge mbele kiuchumi , na tuzidi kuwa Wamoja kama taifa.

Maggid Mjengwa,
Dar es Salaam.
Jumatatu, Februari 6, 2012

Habari kwa Hisani ya Mjengwa Blog

Saturday, February 4, 2012

MGOMO WA MADAKATARI


Ndugu zangu, 

Mgomo wa madaktari wetu ni habari kubwa. Umeingia sasa kwenye wiki ya pili. Hata kama
ungekuwa ni wa siku mbili, bado ungesababisha madhara makubwa kwa nchi. Kwamba
sasa una zaidi ya siku kumi na nne ni balaa kubwa kwa nchi yetu.

Tafsiri yangu; 

Uliopo ni mgogoro kati ya madaktari na Serikali. Na kwenye mgogoro kama huu, siku zote, 
wenye kuathirika zaidi ni wananchi walio wengi.

Ni ukweli, kuwa karibu kila Mtanzania anayeamka asubuhi, ama ni mgonjwa au ana ndugu, 
jamaa au rafiki aliye mgonjwa.

Hivyo basi, kuna mamilioni ya Watanzania wenye kutaabika kila siku na maradhi ya aina mbali mbali. Ni 
Watanzania wenye kutegemea sana huduma ya tiba inayotolewa na madaktari wetu. Na katika nchi
zetu hizi, daktari ni rafiki muhimu sana wa mwananchi.

Ni jambo baya sana, pale Serikali inapoingia kwenye mgogoro na madaktari. Inapoingia 
kwenye mgogoro na marafiki wa wananchi. Hakuna mahali popote duniani wananchi
wakatokea kuwachukia madaktari.

Hivyo basi, ni balaa pia pale Serikali inaposhindwa kumaliza tofauti zake na madaktari wa 
wananchi kwa njia ya mazungumzo na hata kufikia hatua ya madaktari kugoma.

Katika nchi zetu hizi, mganga wa tiba aliyesomeshwa kwa fedha za walipa kodi na kwa miaka 
mingi anahitajika sana. Mganga wa tiba msaidizi anahitajika sana. Na hata kama angelikuwapo
Msaidizi wa Mganga Msaidizi wa tiba , naye angehitajika sana. Vivyo hivyo kwa wakunga wakuu
na wasaidizi, wauguzi wakuu na wasaidizi wao. Wote hao wanahitajika sana.

Na katika nchi zetu hizi, Serikali hazipaswi kufikia hatua ya kuwatisha na hata kuwafukuza kazi 
madaktari. Hilo la mwisho lifanyike tu pale ambapo njia nyingine zote za kumaliza tofauti na
kusuluhisha migogoro na madaktari zitakapokuwa zimeshindikana. Na kwanini ishindakane?

Tufanye nini sasa?
Taarifa kwamba Kamati ya kudumu ya Bunge inayohusika na masuala ya huduma za jamii 
imepanga kukutana na madaktari wetu ni hatua njema na ya busara. Maana, katika mgogoro
huu taarifa zimekuwa zaidi za upande mmoja; upande wa Serikali. Ni wakati sasa pande zote
mbili zikasikilizwa na Kamati hiyo ya Bunge. Ndio, ni wakati pia hata madaktari wetu wakapewa
nafasi tuwasikie.

Huu si wakati wa kufanya ’ propaganda’ za kisiasa kwenye masuala ya afya za wananchi. 
Na hata pale Waziri wa Afya alipokaririwa jana Bungeni akitamka kuwa hali ya huduma za
mahospitalini zimerejea katika hali yake ya kawaida ni mfano wa ’ Propaganda’ za kisiasa
ambazo Watanzania hatuzihitaji kwa sasa. 

Hivi ni hali gani hiyo iliyorejea kwenye kawaida yake
kwenye hospitali zetu baada ya mgomo huu wa madaktari unaoendelea sasa? Kwamba askari
wetu wa Jeshi la Wananchi wamelazimika kwenda kutibu wagonjwa Muhimbili hiyo haiwezi
kuwa ni ’ Hali ya kawaida’. Kwamba madaktari wameripoti lakini hawaonekani mawodini hiyo
haiwezi kuwa ’ hali ya kawaida’. Na kama ni kawaida, hivi ni nini tafsiri ya ’ kawaida’?

Hapa kuna ukweli unaopaswa kusemwa, na si kitu kingine bali ni ukweli. Watanzania tunataka 
kujua; ni kwanini watendaji wa Wizara husika wameshindwa kulitatua suala la madaktari wetu
na hata kutufikisha hapa tulipo? 

Yumkini, kulikuwa na hali ya kuyapuuzia madai ya madaktari
katika hatua za awali. Yawezekana pia watendaji wa Wizara hawakuwa karibu na wawakilishi
wa madaktari hao ili kutoa fursa ya kuongea na kutafuta ufumbuzi wa tatizo. Labda ndio maana
tumefika mahali sasa mgogoro umekomaa na wahusika kuonyesha hali ya kutunishiana misuli.
Kuna mahali kosa limefanyika. Ni wapi?

Ndio hapa, kuwa hata kama Kamati ya Bunge itafaulu kusuluhisha mgogoro huu, bado 
Watanzania tutahitaji iundwe Tume huru itakayochunguza namna watendaji wa wizara husika
walivyolishughulikia suala hili kwa upande wao.

Tume hiyo itusaidie kuupata ukweli mzima ili kama taifa, tujifunze. Na wakati tume kama hiyo 
itakapokuwa ikifanya kazi yake, itakuwa ni busara, kwa watendaji wakuu wa wizara husika
wajiweke pembeni kwa maana ya kujiuzulu ili kupisha uchunguzi huo. 

Kama Tume itabaini kuwa hakukuwa na mapungufu makubwa katika utendaji wao na hususan walivyolishughulikia suala
hili la mgogoro na madaktari, basi, itajulikana hivyo, na wana nafasi ya kurudi tena kwenye
nafasi za utendaji Serikalini. Inahusu umma kurudisha imani yake kwa Serikali yao. Ndio maana
ya umuhimu wa wahusika kupisha pembeni kuruhusu uchunguzi ufanyike. Maana, haitakuwa
busara kuliacha suala hili likapita kama yanavyopita mengine ilihali limegharimu maisha ya
Watanzania.

Na kubwa zaidi kwa sasa, ni kwa pande zote katika mgogoro huu kutambua; kuwa kwa sasa 
mvutano unaoendelea hautatoa mshindi, ni kwa vile, katika kilichotokea na kinachoendelea
kufanyika sasa, sote, kama taifa, tumeshindwa.

Huu ni wakati wa kutanguliza busara na hekima. Tufanye yote, lakini, njia mujarab ya kutanzua 
mgogoro huu uliopo sasa ni mazungumzo katika mazingira ya kuheshimiana, basi.

Mungu Ibariki Tanzania, Mungu Ibariki Afrika. 

Maggid Mjengwa,

Dar es Salaam,
Jumamosi, Februari 4, 2012
KWA HISANI YA MJENGWA BLOG