Ndugu zangu,
Nianze kwanza kwa kuwatakia heri na fanaka za mwaka mpya wa 2012.
Ewe ndugu mwanakijiji wa blogu hii ya Mjengwa, leo tunaumaliza mwaka wa 2011. Hivyo basi, kesho ni siku nyingine tena inayotujia.Ni mwaka mpya. Hivyo, nawe kama utakuwa umejaaliwa siha ya kuyasoma haya. Mshukuru Mungu wako kwa kukujalia hilo.
Katika dunia hii, mwanadamu unaweza kuandaa juu ya nini kifanyike siku ya kifo chako. Lakini, mwanadamu usifikiri sana kuhusu siku yako ya kufa, maana,hujui ni siku gani, lakini itafika siku utakufa, iwe mchana au usiku.
Utakufa ndani ya siku. Ndani ya saa 24. Ndio, utakufa ndani ya mwaka wenye siku 365. Na mauti yakikufika, basi, huna tena utakaloweza kulifanya. Hali yako ya umauti itaachwa kwa wanadamu wenzako. Hivyo, mwanadamu kaa uumize kichwa kufikiri siku unayoishi, na zijazo kama utaishi. Fikiri sasa juu ya utakayoyafanya kwa mwaka huu wa 2012.
Fikiri pia utakayowaachia nyuma wanadamu wenzako. Yale ambayo utapenda ukumbukwe nayo pale watakapotaja jina lako. Maana, si kweli kuwa yote tuyafanyao sasa, mema na mabaya, yatapotea na umauti wetu.
Jiulize; Je, mwaka mpya una maana gani kwangu?
Ndio, nami nimejiuliza swali hilo. Nimetafakari juu ya siku na maana yake kwetu wanadamu. Juu ya mwaka na maana yake kwa mwanadamu.
Najiuliza; siku inakuja au inakwenda? Na mwaka je? Fikra zangu zimenielekeza kwenye kuamini, kuwa wenye kudhani kuwa siku na miaka inakwenda wanakosea. Maana, siku na haziendi wala hazigandi. Siku zinakuja. Vivyo hivyo kwa mwaka. Miaka haendi wala haigandi. Miaka inakuja.
Na usihangaike sana kujiuliza; leo ni siku gani? Lililo muhimu ni kuiona siku. Unaweza hata kuamua uipe siku jina jingine badala ya Jumapili kama ilivyo siku ya leo.
Basi, ewe mwanadamu mwenzangu, kama zawadi, ipokee kwa mikono miwili siku hiyo iliyokujia. Ipokee kwa furaha na si kwa manung’uniko. Mshukuru na mwombe Mungu wako akuongoze katika kuitafuta busara na hekima ya kuitumia vema siku hiyo iliyokujia.
Akuongoze kutenda yalo mema na yenye wingi wa uadilifu. Yale yatakayokuwa na manufaa kwako na kwa wanadamu wenzako. Hivyo basi, kwa jamii unayoishi. Kwa Nchi yako. Usiwe ni mtu mwenye tamaa. Usiwe mbinafsi na mwenye tamaa ya mamlaka.
Na ndugu zangu Wakristo na hata wengine wasio Wakristo wanakitambua kisa cha Essau na Yakobo. Na tafsiri zaweza kuwa nyingi; hii ni ya kwangu. Tunasoma, kuwa Essau na Yakobo walikuwa ni wana wa Isaka.
Essau alikuwa ni mkubwa akifuatiwa na Yakobo. Essau Yule alikuwa ni mwindaji. Naye Yakobo alikuwa akipenda sana kushiriki shughuli za mapishi jikoni akiwa na mama yake.
Biblia inasema, kuwa siku moja Essau alikwenda katika mawindo yake. Alirudi mikono mitupu, hakupata kitoweo. Aliporudi nyumbali Essau alikuwa ni mwenye njaa kali, kwani, aliwinda siku nzima mwituni pasipo kula.
Nyumbani alimkuta Yakobo akiwa amepika dengu. Essau alimuomba Jakobo ampatie bakuli la dengu ili ale na kutuliza njaa yake.
Yakobo alimwambia kaka yake Essau; ” Kama unataka bakuli la dengu, basi, ukubali kuwa mdogo kwangu.” Yaani, Essau akubali kuwa, kuanzia siku hiyo, yeye Yakobo ahesabike kuwa mkubwa (mzaliwa wa kwanza) wa Isaka baba yao, na Essau awe ni mzaliwa wa pili.
Kwa vile Essau alikuwa na njaa sana, alikubali kuwa mdogo kwa Yakobo. Ndipo akapewa bakuli la dengu amalize njaa yake. Naam, tunaona, kuwa njaa ilimfanya Essau auze haki yake ya uzaliwa wa kwanza.
Na ya akina Essau na Yakobo tunayaona sasa. Kuna hata wanaouza haki za Wananchi kwa sababu ya njaa zao. Na wengine si kwamba wana njaa kali hivyo. Ni wenye njaa ya kutaka shibe kama ya mbwa mwitu. Ni watu wenye kuendekeza tamaa.
Na akina Yakobo wa sasa wenye bakuli la dengu baadhi yao ndio hao wanaoitwa wafanyabiashara. Masharti yao ya kutoa bakuli la dengu ni pamoja na kusamehewa kodi au kupewa upendeleo katika kupata tenda mbali mbali. Wamefikia hata kutoa masharti ya kutuchagulia viongozi wetu.
Na nguvu hizo tumewapa wenyewe kwa baadhi yetu kuendekeza njaa na kutaka shibe za mbwa mwitu. Na wenye bakuli la dengu wa siku hizi, hawakupi bakuli la dengu likajaa. Kwamba ule ukashiba. La, watakupa dengu kiduchu ili urudi tena kuomba bakuli lingine. Uwe tegemezi kwao.
Ndugu zangu,
Kuna wengi mlio kwenye jiko lenye giza huku mkiwa na njaa kali. Mnachohitaji kwanza ni ukombozi wa kifikra . Ukombozi huo utawapelekea kwenye kuepuka kufa na njaa. Kuepuka kuwa watumwa kwenye nchi yenu mliyozaliwa. Kwenye ardhi ya mababu zenu. Anzeni sasa kuuwasha moto. Moto huo utawapa pia mwanga kwenye jiko hilo lenye giza nene.
E nendeni mkayatafute majani makavu. Kisha muyaweke katikati ya mafiga. Tieni moto kiberiti muyawashe. Yakishawaka, anzeni taratibu kuweka vijiti na vibanzi vikavu juu yake. Na vitakaposhika moto, endeleeni kuweka kuni kubwa huku mkipulizia.
Moto utakaowaka hapo hautazimika kirahisi. Utawapa shibe ya boga au muhogo. Utawapa mwanga pia. Ni mwanga wa ukombozi wa kifikra na kiuchumi. Heri ya Mwaka Mpya kwenu nyote.

Maggid Mjengwa,
Bagamoyo
Desemba 31, 2011