WHATEVER YOUR ARE BE A GOOD ONE;

A nation that is afraid to let its people judge the truth and falsehood in an open market is a nation that is afraid of its people. John F. Kennedy

“Taifa letu – taifa lolote – ni zuri na mahali pazuri pa kuishi kama raia wake watalifanya liwe hivyo. Uongozi wake unaweza kuwa mzuri, mbaya au usiojali lakini kama watu wake wameamka (ki-elimu?) na wanajitambua, haitachukua muda mrefu kuwakilisha mtazamo wa jamii na kubadili mawazo na matumaini ya taifa.” Julius Kambarage Nyerere


Thursday, June 18, 2015

DK SHEIN AKICHUKUA FOMU KUOMBA RIDHAA YA KUGOMBEA URAIS ZANZIBAR


Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein akionesha mkoba wa wenye fomu kuomba ridhaa kwa Chama cha Mapinduzi kumteuwa kuwa mgombea Urais wa Zanzibar baada ya kukabidhiwa Fomu hizo katiuka Ofisi ya CCM Kisiwandui Mjini Unguja leo
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein akiwapungia mkono Wanachama wa CCM waliofika Viwanja vya Jengo la Ofisi ya CCM Kisiwandui Mjini Unguja leo wakati alipofika kuchukua fomu kuomba ridhaa kwa Chama cha Mapinduzi kumteuwa kuwa mgombea Urais wa Zanzibar akifuatana na Mkewe Mama Mwanamwema Shein
Viongozi wa Chama cha Mapinduzi waliofika katika ukumbi wa Ofisi ya CCM Kisiwandui Mjini Unguja wakisherehekea wakati Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein alipokwenda kuchukua fomu kuomba ridhaa kwa Chama cha Mapinduzi kumteuwa kuwa mgombea Urais wa Zanzibar katika Ofisi ya CCM Kisiwanndui Mjini Unguja leo
Viongozi wa Chama cha Mapinduzi waliofika katika ukumbi wa Ofisi ya CCM Kisiwandui Mjini Unguja wakimsikiliza Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein alipozungumza nao baada ya kuchukua fomu za kuomba ridhaa kwa Chama cha Mapinduzi kumteuwa kuwa mgombea Urais wa Zanzibar katika Ofisi ya CCM Kisiwanndui Mjini Unguja leo
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein akionesha Fomu za kuomba ridhaa kwa Chama cha Mapinduzi kumteuwa kuwa mgombea Urais wa Zanzibar kwa Viongozi wa Chama cha Mapinduzi waliofika katika ukumbi wa Ofisi ya CCM Kisiwandui Mjini Unguja leo alipokuwa akizungumza nao baada ya kuchukua fomi hizo (kushoto) Makamo wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi,(kulia) Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Vuai Ali Vuai
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein alipozungumza na Viongozi wa Chama cha Mapinduzi waliofika katika ukumbi wa Ofisi ya CCM Kisiwandui Mjini Unguja leo baada ya kuchukua fomu za kuomba ridhaa kwa Chama cha Mapinduzi kumteuwa kuwa mgombea Urais wa Zanzibar. Picha na Ikulu, ZNZ(Muro)

source: mjengwa blog

Wednesday, June 17, 2015

Waziri Mmarekani amuuliza JK utitiri wa wagombea urais

Rais Jakaya Kikwete akiagana na Makamu wa Rais wa zamani wa Sudani ya Kusini (kushoto),  Riek Machar Teny Dhurgon baada ya kufanya naye mazungumzo mafupi walipokutana jijini Johannesburg, Afrika ya Kusini, juzi wakati wa Mkutano wa 25 wa Kawaida wa  Marais na Wakuu wa Nchi za Umoja wa Afrika (AU), . Kulia ni mke wa Rais Mama Salma Kikwete. Picha na Ikulu 
Na Waandishi Wetu
Dar/Mikoani. Waziri Mdogo wa Mambo ya Nje wa Marekani anayeongoza Kitengo cha Masuala ya Afrika, Linda Thomas-Greenfield amemuuliza Rais Jakaya Kikwete iwapo ana mtu wake katika orodha ndefu ya makada waliojitokeza kuomba kuwania urais kwa tiketi ya CCM.
Waziri huyo aliuliza swali hilo usiku wa kuamkia Jumatatu (Juni 14, 2015) mjini Johannesburg, Afrika Kusini wakati anazungumza na Rais Kikwete kutokana na wanachama wa CCM 35 kujitokeza kuchukua fomu za kuwania urais.
Viongozi hao walikuwa wanahudhuria Mkutano wa 25 wa Umoja wa Afrika (AU) uliofanyika, kwa siku mbili, kwenye Kituo cha Mikutano cha Sandton Convention jijini Johannesburg, Afrika Kusini na kumalizika jana.
Makada hao wa CCM wameibua upinzani mkali kwenye mbio za urais na hadi sasa hakuna dalili za mtu yeyote kuwa ana nafasi kubwa ya kupitishwa, hali ambayo imesababisha vyombo vya habari kubashiri kuwa mteule wa CCM anajulikana kwa viongozi wa juu wa chama hicho tawala.
Wakati nchi ikijiandaa kupata kiongozi mpya atakayeongoza Serikali ya Awamu ya Tano, mbio za urais ndani ya CCM zimevutia idadi kubwa ya wanachama ambayo haijawahi kutokea kabla na baada ya kurejeshwa kwa mfumo wa vyama vingi nchini mwaka 1992 baada ya watu 35 kuchukua fomu hadi sasa.
Mwaka 1995, wanaCCM waliojitokeza kutaka kumrithi Rais Ali Hassan Mwinyi walikuwa 15 na mwaka 2005 waliojitokeza kutaka kumrithi Rais Benjamin Mkapa walikuwa 11.
Taarifa ya Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais, Ikulu ilisema jana kuwa mwanzoni tu mwa mazungumzo baina ya viongozi hao, Linda alimuuliza Rais Kikwete, “Je, unaye mgombea yeyote ambaye unampendelea miongoni mwa utiriri wa wagombea”.
Baada ya swali hilo, kwa mujibu wa taarifa ya Ikulu, Rais Kikwete alijibu, “Sina mgombea ninayempendelea. Wagombea wote ni wa kwangu, ni wa chama changu, isipokuwa ninayo kura moja ambayo kwa mujibu wa taratibu za haki katika chama chetu nitaitumia katika vikao mbalimbali”.
Kuhusu utiriri wa wagombea, Rais Kikwete alisema wingi wa wagombea ni jambo zuri kwa CCM.
“Hiki ni chama kikubwa. Wingi unatupa nafasi ya kujadili kwa nafasi nani awe mgombea wetu. Isitoshe, tunaona wagombea wengi zamu hii kwa sababu ya wigo mkubwa wa uhuru ambao umejengeka katika nchi yetu katika miaka ya karibuni.
“Vile vile, wingi wa wagombea unathibitisha mafanikio yetu katika miaka 10 iliyopita kwa sababu tungeshindwa, watu wangeogopa kujitokeza kugombea nafasi hiyo.”
Rais Kikwete alisema hana tatizo na wingi wa wagombea kwa sababu haiwezekani kuwazuia watu kugombea nafasi hiyo kwa sababu ni haki yao.
Vile vile, alisema wingi wa wagombea zamu hii ni jambo zuri na pia ni ushahidi wa kiasi cha uhuru ambao umejengeka ndani ya chama na ni uthibitisho kuwa uongozi wa Tanzania katika miaka 10 iliyopita umekuwa wa mafanikio.
Uchaguzi mkuu wa Marekani utafanyika mwakani na kwa mujibu wa taratibu zao, mchakato huanza mwaka mmoja kabla na wagombea hupatikana Juni ya mwaka wa uchaguzi.
Hadi sasa, makada wanne wa chama cha Democrats, ambacho kimeshika hatamu, wamejitokeza kuwania urais, wakati katika chama cha Republican, ambacho kina nafasi kubwa ya kushika madaraka mwakani baada ya kukaa nje kwa miaka 10, kuna makada 12 waliojitokeza.
CCM iteue kwa staili ya Papa
Katika hatua nyingine, mbunge wa Ngara (CCM), Deogratias Ntukamazina ameitaka Kamati Kuu ya CCM kutumia mfumo wa Vatican wa kujifungia na kuomba siku saba kabla ya kumpata Papa wakati itakapokutana kuteua mgombea urais wa chama hicho baadaye mwezi huu.
Katika mchakato wa kumchagua Papa, Makardinali kutoka sehemu mbalimbali duniani, hukutana kwenye mji wa Vatican na kujifungia katika mkutano wao (Conclave) wakiomba ili apatikane Papa na baada ya kukamilisha mchakato huo, moshi mweupe huonekana juu ya jumba la mkutano kuashiria kukubalika kwake kwa Mwenyezi Mungu.
“Mimi siwanii tena (ubunge), lakini ninachosema, tuache ushabiki… ninaondoka, lakini nina ushauri kwa Kamati Kuu na Halmashauri Kuu. Kwanza ninawapongeza waliojitokeza kuwania urais lakini siyo yule msanii wa darasa la saba.
“Tuombe Mungu atupe Rais mzuri, anayependa watu, anayependa maendeleo ya watu, lakini na Kamati Kuu muanze kuomba Mungu kama anavyotafutwa Papa. Makardinali wanajifungia siku saba, wanaomba, wanaomba na ninyi ombeni. Sasa na sisi tusishabikie, tuache vikao vitaamua,” alisema Ntukamazina wakati akichangia mjadala wa bajeti bungeni.
Membe aibukia kwa Msuya
Jana wagombea wa CCM waliendelea na safari ya kutafuta wadhamini huku Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe aliibukia kwa nyumbani kwa Waziri Mkuu wa zamani, Cleopa Msuya.
Membe alifika nyumbani kwa Msuya eneo la Usangi, Mwanga mkoani Kilimanjaro na kufanya naye mazungumzo akitokea mkoani Tanga ambako aliahidi kuwa akibahatika kuingia Ikulu, kwanza atashughulika na bandari ya Tanga.
Katika mazungumzo yao, Msuya alisema anamuunga mkono Membe katika harakati zake za kugombea urais kwa kuwa anakidhi vigezo vilivyotajwa na Makamu Mwenyekiti wa CCM, Philip Mangula.
Msuya alisema ana matumaini CCM itamteua Membe kwa kuwa ni mgombea pekee ambaye hajawahi kukumbwa na kashfa na amekidhi sifa zinazohitajika.
Msuya alisema chama hicho hakipaswi kumchagua mgombea mwenye madoadoa ya ufisadi na uchafu kwa kuwa mgombea wa aina hiyo hatawatendea haki Watanzania.
Alisema katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi wa ngazi za madiwani, wabunge na rais, chama kinapaswa kuwatanguliza watu wenye sifa na vigezo ili kupata viongozi bora watakaowatumikia wananchi.
“Kama kweli Taifa linawachukia mafisadi na wenye kila aina ya madoadoa, chama hakipaswi kuwapitisha viongozi wa aina hiyo kwa kuwa
wataendeleza ufisadi huku Watanzania wakiendelea kuteseka,” alisema Msuya
“Kama tunachukia ufisadi na matendo machafu haya yanayoendelea kufanywa na baadhi ya watu katika Serikali yetu basi mgombea mwenye madoadoa hataweza kuwatendea haki Watanzania kwani wananchi wanahitaji mtu safi na asiyekuwa na aina yoyote ya uchafu,” alisema Msuya.
Pinda atikisa kwao
Mkoani Katavi; Waziri Mkuu Mizengo Pinda ameanza mbio za kusaka wadhamini jimboni kwake Katavi ambako alipokewa kwa maandamano na kuchangiwa Sh1 milioni za kumsaidia kuzunguka katika mikoa mingine kutafuta wadhamini.
Pinda maarufu kama “Mtoto wa Mkulima” alipokewa kwa mabango yaliyoandikwa “Pinda siyo fisadi… ni mtoto wa mkulima… karibu nyumbani… wewe ndiye rais ajaye”, na alisindikizwa kwa maandamano yaliyowafanya askari kuwa na wakati mgumu kudhibiti ulinzi.
Baada ya kupata wadhamini 9,141 katika tarafa mbalimbali za mkoa wa Katavi, Pinda aliwashukuru na kueleza kuwa tukio hilo ni la kihistoria na kuwaomba wananchi waendelee kumwombea ili aweze kupata ridhaa ya chama chake na hatimaye kuwa rais.
Wasira na uchapakazi
Mkoani Njombe, Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Steven Wasira amesema uchapakazi na uaminifu wake ndio uliofanya kila Rais aliyepita ahitaji kufanya naye kazi.
Wasira, ambaye pia ni mbunge wa Bunda alisema hayo jana wakati akitafuta wadhamini katika mkoani Njombe. Alisema asingekuwa mwaminifu, angekuwa ameshawekwa pembeni kama ambavyo baadhi ya mawaziri wamefanywa.
“Nimekuwa sehemu ya uongozi wa Taifa letu kwa miaka kadhaa, nimeanza na Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, akaja Mzee Ali Hassan Mwinyi, Benjamin Mkapa na sasa Jakaya Kikwete, kwa hiyo ni walimu wangu wanne, uzoefu nilioupata kutoka kwao ni shule tosha kwangu ya kuliongoza Taifa hili,” alisema Wasira.
Bilohe na siri ya urais
Kada wa CCM anayewania kuteuliwa na chama hicho kugombea urais, Edephonce Bilohe amesema hatishiki wala kuwaogopa wagombea wanaonunua watu kwa nguvu ya fedha kwa kuwa uongozi ni tunu kutoka kwa Mungu.
“Natambua kwamba nagombea nafasi hii kubwa zaidi nchini nikishindana na wasomi na matajiri, lakini kamwe sitishwi na hawa wagombea wanaojidai kuhonga viongozi na watu wengine ili wawaunge mkono,” alisema Bilohe.
“Tangu nikiwa mdogo tulikuwa tunaambiwa kwamba CCM ni chama cha wakulima na wafanyakazi, ndiyo maana mimi nikiwa mkulima katika Kijiji cha Muzye na Mtala niliamua kwa moyo wangu wote kugombea urais ili niwawakilishe maskini wenzangu ambao ndio wengi katika jamii na sina shaka wataniunga mkono katika harakati zangu za kuingia Ikulu kuongoza Taifa,” alisema.
Kuhusu migogoro ya wakulima na wafugaji, alisema: “Ni aibu nchi ya wastaarabu kama Tanzania, inayoongozwa na viongozi wasomi bado tunashuhudia mapigano ya wakulima na wafugaji wakigombea maeneo ya kulima na kuchungia mifugo.
“Nchi yetu ina ardhi kubwa isiyokaliwa na watu na haijawahi kutumika tangu dunia iumbwe, iweje sasa watu wauane kwa ajili ya ardhi? Hili nitalikomesha.”
Imeandikwa na Ibrahim Bakari, Habel Chidawali, Kibada Ernest, Burhani Yakub, Antony Kayanda na Rehema Matowo.
source: mwananchi

Friday, June 5, 2015

Maalim Seif ‘kidedea’, kuwania urais Zanzibar

  Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi CUF,Maalim Seif  Sharif Hamad. 
Na Mwinyi Sadallah

Zanzibar. Chama cha Wananchi CUF kimempitisha katibu mkuu wake, Maalim Seif Sharif Hamad kuwa mgombea urais wa Zanzibar kwa mara ya tano.
Pia, CUF imewarudisha baadhi ya wagombea wa nafasi za ubunge na uwakilishi walioanguka katika kura za maoni za majimboni.
Maalim Seif amepitishwa na CUF kuwania nafasi hiyo kwa mara tano tangu kurejeshwa kwa mfumo wa siasa za ushindani na mara moja akiwa CCM mwaka 1984 wakati alipochuana na Marehemu Idirisa Abdulwakili.
Akizungumza na wanahabari ofisini kwake Vuga mjini hapa, mkurugenzi wa mipango na uchaguzi wa CUF, Omar Ali Shehe alisema kwamba, Maalim Seif amechaguliwa baada ya kupata ushindi wa asilimia 100 kwa kuzoa kura zote 56 za wajumbe wa Baraza Kuu.
Alisema wajumbe wa Baraza Kuu la Taifa walilazimika kupiga kura ya “Ndiyo” na “Hapana” kutokana na kuwa na mgombea mmoja na kura zote zilimuunga mkono mwanasiasa huyo mkongwe na hakuna kura iliyoharibika.
Shehe aliwataja wagombea waliorudishwa kuwa ni mbunge wa Mtambile, Masoud Abdalla Salim na mwakilishi wa Jimbo la Kojani, Hassan Hamad Omar huku kukiwa hakujapatikana kwa wagombea kwenye majimbo ya Raha Leo, Makunduchi na Mtambwe kutokana na sababu mbalimbali ikiwamo ya kukatiwa rufaa pamoja na Baraza kuu kutoridhika.
Wagombea waliopitishwa kugombea ubunge na uwakilishi ni Ismail Jussa Ladhu (uwakilishi) na Ali Saleh Abdalla (ubunge) wa Jimbo la Jangombe, Ali Haki Mwadini (uwakilishi) na Mohamed Yussuf Maalim (uwakilishi).
Katika Jimbo la Kikwajuni, Moh’d Khalfan Sultani (uwakilishi) na nafasi ya ubunge imeachiwa Chadema.
Jimbo la Chumbuni ni Maulid Suleiman Juma (uwakilishi) na Omar Ali Khamis (ubunge), Jimbo la Kwamtipura Amina Rashid Salum (uwakilisihi) na Abdi Seif Hamad (ubunge), Jimbo la Magomeni Yussuf Idrisa Mudu (uwakilishi ) na Ahmed Khamis Hamad (ubunge).
Jimbo la Mpendae ni Ali Hamad Ali (uwakilishi) na Omar Moh’d Omar (ubunge), Jimbo la Amani ni Khamis Rashid Abeid (uwakilishi) na Khamis Silima Ame (ubunge) . Jimbo la Kwahani Hassan Juma Hassan (uwakilishi) na Khamis Mussa Haji (ubunge) Magomeni, Abdilahi Jihad Hassan (uwakilishi) na Saleh Mohamed Saleh (ubunge).
Jimbo la Bububu, Waziri wa Miundombinu na Mawasiliano, Juma Duni Haji (uwakilishi) na Juma Khamis Juma (ubunge). Jimbo la Mfenesini ni Saleh Khamis Omar (uwakilishi) na Hassan Othman Makame (ubunge) huku Jimbo la Mtoni ni Waziri wa Biashara na Masoko, Nassor Ahmed Mazrui (uwakilishi) na Ali Ame Ali (ubunge).
Katika jimbo la Dole amepitishwa Yussuf Omar Muhine (uwakilishi) na Khamis Msabah Mzee (ubunge) Jimbo la Dimani ni Mohamed Hashim Ismail (uwakilishi) na Khalid Said Suleiman (ubunge) na Jimbo Kiembesamaki ni Waziri wa zamani SMZ Mansour Yussuf Himid (uwakilishi) na Mohamed Nassor Mohammed (ubunge), Mwanakwerekwe ni Ussi Juma Hassan (uwakilishi) na Ali Salum Khamis (ubunge). wakati Jimbo la Fuoni Suleiman Simai Pandu (Uwakilishi) na Mohamed Juma Aminia (Ubunge) na jimbo la Nungwi Hassan Jani Masoud (Uwakilishi) na Yussuf Haji Khamis (Ubunge).
Wengine ni Nahoda Khamis Haji (Uwakilishi) jimbo la Matemwe na Dunia Haji Pandu (Ubunge ) Jimbo la Mkwajuni Haji Kesi Haji (Uwakilishi) na Khamis Masoud Nasor (Ubunge).
Katika jimbo la Chaani Khamis Amour Vuai (Uwakilishi) na Khatib Ali Juma (Ubunge) wakati jimbo la Tumbatu Makame Haji Makame (Uwakilishi) na Rashid Khamis Rashid (Ubunge) pamoja na jimbo la Donge Suleiman Ahmed Sleiman (Uwakilishi) na Kombo Mohamed Kombo (Ubunge)
Wagombea wengine waliteuliwa ni Zahran Juma Mshamba (Uwakilishi) Jimbo la Bubwini na Mohamed Amour Mohamed (Ubunge) Jimbo la Kitope Hassan Khatib Kheir (Uwakilishi) na Mwinshaha Shehe Abdalla (Ubunge).
Jimbo la Uzini Asha Simai Issa (Uwakilishi) na Adam Ali Wazir (Ubunge) Khamis Malik Khamis (Uwakilishi) Jimbo Koani Shaaban Iddi Ame (Ubunge)na jimbo la Chwaka Arafa Shauri Mjaka (Uwakilishi ) pamoja na Ali Khamis Ame (Ubunge).
Wagombea wengine Asha Abdu Haji (Uwakilishi) Jimbo la Muyuni na Baswira Hassan Suleiman (Ubunge) wakati nJimbo la Tumbe Mohamed Hemed (Uwakilishi) na Rashid Ali Abdalla (Ubunge) pamoja na Jimbo la Micheweni Subeit Khamis Faki (Uwakilishi) na Haji Khatib Kai (Ubunge).
Wengine Issa Said Juma Jimbo la Konde (Uwakilishi) na Khatib Said Haji (Ubunge) pamoja na Waziri wa Katiba na Sheria Abubakar Khamis Bakar Jimbo la Mgogoni (Uwakilishi) na Juma Kombo Hamad (Ubunge) wakati Jimbo la Wete DK Suleiman Ali Yussuf (Uwakilishi) na Mbarouk Salum Ali (Ubunge).
Hamad Masoud Hamad Jimbo la Ole (Uwakilishi) na Rajab Mbarouk Mohamed (Ubunge) pamoja na Waziri wa Habari Utamaduni, Utalii na Michezo Said Ali Mbarouk Jimbo la Gando (Uwakilishi) na Othman Omar Haji (Ubunge).
Katika jimbo la Mtambwe Mwakilishi hajapatikana kutokana na matokeo ya kura ya maoni kukatiwa rufaa lakini Khalifa Mohamed amepitishwa nafasi ya (Ubunge) na Jimbo la Kojani Hassan Hamad Omar (Uwakilishi) na Hamad Salum Maalim (Ubunge).
Jimbo la Chake Chake Omar Ali Shehe (Uwakilishi) na Yussuf Kaiza Makame (Ubunge) wakati Jimbo la Chonga Khamis Faki Marango (Uwakilishi) na Moh’d Juma Khatib (Ubunge) Jimbo la Ziwani Mohamed Ali Salum (Uwakilishi) na Ahmed Juma Ngwali (Ubunge)
Wengine Khalifa Abdalla Ali Jimbo la Wawi (Uwakilishi) na Waziri wa zamani wa Utalii katika Serikali ya Jamhuri ya Muungano Juma Hamad Omar (Ubunge) na jimbo la Chamabani Mohamed Mbwana Hamad (Uwakilishi) Yussuf Salim Husein (Ubunge) wakati Jimbo la Kiwani Hija Hassan Hija (Uwakilishi) na Abdalla Haji Ali (Ubunge).
Katika Jimbo la mkanyageni Tahir Aweis Mohamed (Uwakilishi) na . Mohamed Habibu Juma Mnyaa (Ubunge) na Seif Khamis Mohamed Jimbo la Mkoani (Uwakilishi) na Ali Khamis Seif (Ubunge) wakati Jimbo la Mtambile Abdalla Bakar Hassan (Uwakilishi) na Masoud Abdalla Salim (Ubunge)
Wagombea hao kwa tiketi ya Chama cha wananchi CUF ndiyo wanatarajia kuchuana na vyama vingine vitakavyosimamisha wagombea katika uchaguzi wa mwaka huu.

chanzo: mwananchi

Wednesday, June 3, 2015

LIGI YA KUINGIA IKULU IMEANZA TANZANIA





SIFA YA MCHEZAJI MAHIRI ANAYETAKIWA IKULU:
  •  MWADILIFU
  •  MWAJIBIKAJI
  •  MKWELI
  •  MTETEZI WA AMANI
  •  RAFIKI NA MTETEZI WA WANYONGE
  •  SHUPAVU KATIKA MAAMUZI
  •  AWE TAYARI KUTUVUSHA KAMA TAIFA KUTOKA KATIKA DIMBWI LA UMASIKINI
  • MTU WA WATU
  •  MKUZAJI WA DEMOKRASIA
  •  MWOGOPA MUNGU
  •  ANAYEWEZA WAKEMEA RAFIKI ZAKE MAFISADI

Taifa letu linaelekea katika uchaguzi wa viongozi ambao kupitia vyama vyao vya siasa wataunda serikali ya kuongoza nchi yetu kwa kipindi cha miaka mitano baada ya uchaguzi wa October 2015.
Mimi jicho langu kubwa ni kwa kiongozi Yule ambaye atashika hatamu ya kuongoza Taifa letu na ambaye atahamishia makazi yake IKULU.

 
Kama taifa ni wakati mzuri umewadia sasa tuweze kumchagua mtu makini, mbunifu, mwaminifu, mwadilifu na mzalendo wa kweli kwa wananchi wanyonge na masikini wa Taifa letu.Kiongozi ambaye tunamwitaji lazima atambue kuwa kuwa wananchi wana haki ya kupata chakula bora, mavazi bora, malazi bora – maisha bora.


Akumbuke kuwa wanaompeleka Ikulu ni wananchi wa Jamuhuri ya muungano wa Tanzania na sio marafiki wachache wenye pesa. Na ajue kuwa anapochaguliwa kuongoza, ajuwe anabeba jukumu la kubadilisha hali za watu kuwa nzuri awe tayari kuongoza kwa kuonyesha njia awe ni mfano wa uwajibikaji.
 

Kiongozi tutakaye mchagua lazima awe na tabia ya kuongoza kwa kutofikiria zaidi maslahi binafsi wazo hili liwe mwiko. Tutataka atumie ustadi wa uongozi ambao utasimamia haki za waoongozwa; wanyonge. Wajikumbushe kuwa kupewa uongozi ni kuchukua ahadi ya kutenda kwa haki.

Hatuki kumchagua kiongozi ambaye baada ya kuchaguliwa ataigeuza ikulu kuwa Ni pango la wizi, rushwa, uonevu, unyonyaji wa rasilimali za watanzania kwa masilahi binafsi pamoja na marafiki wachache.  Tunahitaji kiongozi ambaye uadilifu kwake utakuwa ni sehemu ya maisha yake ya kila siku bila kujali au kupendelea mtu au kikundi cha watu au vile vile awe na uwezo wa kuwajibisha viongozi watakao kuwa chini yake wanapotenda kinyume na taratibu na sheria zilizowekwa.

 

Mwalimu Nyerere aliandika miongozo mizuri katika Azimio la Arusha akisema kwamba ili tuendelee tunahitaji mambo matatu: Watu, Ardhi, Siasa Safi na Uongozi Bora. Alitambua mchango wa mambo hayo katika maendeleo ya mwanadamu. Kiongozi wetu tunataka aongoze katika misingi hiyo.

Kiongozi lazima ajue kuwa hakuna mamlaka isiyotoka kwa Mungu. Zaidi ya yote Mungu anaangalia sana nani ataongoza watu wake wateule. Tukiangalia katika historia ya dunia sehemu nyingi, Viongozi wa taifa walipoongoza kufuatana na mapenzi ya Mungu nchi yote ilisitawi na kubarikiwa katika njia njia nyingi. Walipomsahau Mungu kupitia rushwa na ufisadi na dhuluma shida na dhiki zilianza.



Kama Mungu ndiye anayewapa viongozi mamlaka ina maana ya kwamba kila kiongozi atajibu mbele za Mungu jinsi alivyoongoza. Kiongozi anayefahamu kwamba atatoa hesabu kwa Mungu anahakikisha kwamba mwenendo wake unapatana na Neno la Mungu.

Itakuwa jambo bora tuweze kupata viongozi ambao kwa kweli nao watakuwa bora katika kuongoza Taifa letu kuelekea kwenye maisha bora kwa kila mtanzania. kiongozi  kuongoza kwa uwajibikaji; kuonyesha uzalendo na kuwa mfano bora kwa viongozi wengine.Pengine katika msingi huu tutahitaji kiongozi ambaye anauelewa mpana wa kuelewa shida za wananchi mwenye UWEZO wa kufikiri kwa usahihi, kuamua kwa usahihi na kutenda kwa usahihi wakitambua dhamana ya uongozi ambao taifa linampa. Kwa hivyo tutahitaji  RAIS pamoja na mambo mengine awe na UWEZO kuongoza kwa usahihi. 

Vile vile tunahitaji viongozi wajao katika serikali zetu mbili wawe ni watu wa WATU; viongozi ambao wataweza kuona matatizo ya wananchi wao ni yao na yanawakera wanawanyima usingizi, yana wafanya waongeze nguvu ya uwajibikaji wa kusimamia rasilimali za Taifa. Nasi kama wananchi tuwe na uwezo wa kuwapima kwa watakacho kifanya wakiwa madarakani.

Pengine tutahitaji kidogo aina ya viongozi wetu wawe wakali japo sio sahihi kutumia msemo huu lakini wakati mwingine ile tuweze kupiga hatua ya maendeleo tutahitaji viongozi wenye mawazo ya  uwajibikaji chanja; ili tuweze kubadilisha kidogo maadili ya utendaji kwa  Watanzania; Tunahitaji  Maraisi katika serikali zetu mbili ambao wanaweza  kuwawajibisha mara moja watendaji wake ambao wanashindwa kuwajibika, tuwapate viongozi ambao wanaweka pembeni huruma ambazo hazina msingi kwa Taifa;
 


Nafikiri itakuwa ni jambo la busara kama sisi kama watanzania na wapiga kura tukiweza kuepuka tabia ya kuwachagua viongozi wetu kwa  Mazoea, Mkumbo na kwa kutumia Hisia na mapenzi binafsi juu ya wagombea. Nafikiri umefika wakati tuwachagua viongozi wetu kwa upeo wao wa kuona mambo mbalimbali nauwezo wao wa uongozi hapa nazungumzia uzoefu wa kiongozi kabla ya kuchaguliwa kuwa rais je amefanikiwa kwa kiasi gani katika idara ambayo amewahi kuongoza?

kama taifa tunafahamu kuwa taifa letu bado linaogelea sana katika tope nzito la matumizi mabaya ya rasilimali ya Taifa Rushwa na Ufisadi basi tunahitaji Rais ambaye analiona hili kuwa ni tatizo na linahitaji utatuzi wa haraka. Lazima tukubali kuwa mabadiliko yoyote ya kisiasa, kijamii na kiuchumi yenye kulenga kuletea faida wananchi walio wengi hayawezi kufanikiwa bila ya kutokomeza rushwa na ufisadi. Kiongozi wetu aweze kuliona hili na kuwa tayari kupambana nalo akiamini kuwa Tanzania rushwa imeshaota mizizi, umepelekea mamilioni ya watanzania kupoteza matumaini na hali zao za maisha lakini kupitia yeye ataweza kulitatua tatizo hili na kuwachukulia sheria wale wote ambao wamehusika katika uchafu huu,
 

Tunahitaji kiongozi ambaye ataweza kuyatekeleza kwa vitendo manemo haya ya Mheshimiwa Yusuph Makamba “maendeleo ya Watanzania yataletwa na wao wenyewe, kwa kufanya kazi. Watanzania wamekuwa wavivu wa kufanya kazi na kwamba kila kitu wanategemea kitafanywa na serikali … Watanzania wataendelea kulia umaskini kwa kuwa hatuna tabia ya kushirikiana na kufanya kazi,”. Kauli hii ni nzito kiongozi wetu anayetaka kuongoza taifa hili lazima awe tayari kuwaeleza wananchi bila kuogopa kukosa kura katika kipindi kingine cha uchaguzi.

 Daima tunapofikiria kuwachagua viongozi wa juu wa Taifa letu tunayakumbuka maneno ya Baba wa Taifa  Mwalimu Nyerere aliwahi sema kuwa kazi ya urais ni ngumu na inahitaji busara na kuchukua maamuzi magumu, ili kuweza kutimiza haki wananchi wanyonge “ walala hoi ”; aliendelea kushauri kuwa “Ole wale wanaokimbilia Ikulu, wanakimbilia nini, Ikulu hakuna biashara ya kufanya, Ikulu ni mahali patakatifu na kama kuna mtu anadhani kuwa kukaa Ikulu ni raha basi angeniuliza mimi katika kipindi cha miaka 21 niliyokaa Ikulu nimefanya biashara gani,Ikulu ni mzigo mzito”
 

Mwandishi Nyenyembe aliwahi andika kuwa “Kwa maana hiyo mtu anapoamua kuulilia urais,urais sio pambo la nchi,urais ni jalala, urais ni chumba cha kuhifadhia maiti,urais ni njaa,urais ni magonjwa,urais ni bakuli la kukingia machozi ya watu wanyonge wanaolia kila siku wakihitaji msaada na kama hawapati anayetazamwa hapo ni rais”

Katika demokrasia wananchi ndio wenye dhamana na uwezo wa mwisho wa kumrejesha mwanasiasa kuendelea kuhozi madaraka; pamoja na umaarufu wake, uadilifu na utaalam katika kushughulikia maswala ya siasa bila ridhaa ya mwananchi sio rahisi kurejea madarakani; 
 


Hebu tuanagalie historia ya vyama vingi na chaguzi za Zambia zinaainisha kwa ukomavu wa demokrasia ndani ya Zambia wananchi ndio wenye sauti ya mwisho wananchi wa Zambia wanapima na kuamua kulingana na utendaji wa viongozi wao na sio ushabiki wa vyama vyao;wamejitahidi sana kuweka nchi mbele vyama baadae.

Tatizo la kushabikia sana vyama ndilo linaloponza sana maendeleo ya nchi nyingi za kiafrika; wananchi wanakumbatia zaidi chama na sio utendaji wa viongozi wa vyama vyao;
 


Kama wananchi tunatakiwa kuanza kuangalia upya maamuzi yetu dhidi ya viongozi wetu; tunahitaji viongozi waadilifu na viongozi wa namna hii  wataweza kuchukua hatua kwa maslahi ya jamii kwa manufaa ya wote, na wanaweza kubaki madarakani kwa muda mrefu iwezekanavyo kulingana na utaratibu wa nchi husika na kukendelea kukubalika kwako kwa masilahi ya wengi; Katika mfumo wa kidemokrasia wa serikali, ambapo nguvu ya utawala ina inapatika upya kila baada ya miaka mitano na wananchi ndio wenye dhamana ya kuwarejesha madarakani.

Nchi ya Zambia imetufundisha kuwa  hakuna kiongozi anayemiliki watu, hakuna chama chenye hatimiliki ya kuwa na kundi la wananchi kama itakuwa hivyo basi kuna tatizo na wananchi katika nchi hiyo; wananchi mara zote wanategemea na wanataka  mabadiliko makubwa ya kiuchumi hawahitaji propaganda za chuki, wanahitaji kufaidi raslimali zao  wazambia walikuwa wanashangaa utajiri wote unaotokana na shaba unakwenda wapi? Pale ambapo hawakuridhika hawakuwa na papara walisubiri tu wakati ulipofika walimweka pembeni kiongozi na kumpa dhamana kiongozi mwingine. Lazima tukubali kuwa katika nchi zilizopo kusini mwa Afrika  Zambia ni moja ya changamoto za mabadiliko ya kisiasa:

Maamuzi ya wananchi katika awamu tofauti Zambia umeendelea kuwashangaza viongozi walioko madarakani kuanzaia enzi  Kaunda, pamoja na ukongwe wake wa kutawala kwa miaka 27 hadi awamu ya Banda; Kiini cha msukumo huu nini? Wananchi wanatamani kupata maisha bora; na kuwa viongozi wenye kiwango cha juu kabisa cha uadilifu kuweza kuwatumikia wananchi na kuleta maendeleo sio kwa nadharia bali vitendo;
 


Viongozi wetu wa vyama vya siasa wamesahau kuwa, Kimsingi, raia huzaliwa wakiwa huru dhidi ya mikingamo ya kijamii, kwa lugha ya kitaalamu tabula rasa. Lakini mikingamo hii ya kijamii huingizwa katika fikra za wananchi kupitia itikadi na elimu ya siasa katika vyama ambavyo wanafuata; na wakati mwingine hata kupitia shule na sehemu za ibada.

Cha ajabu haitoshi kuivuruga jamii peke yake tumeona na tunaendelea kuona kuwa viongozi wetu wa kisiasa hapa nchini wamekuwa wakigombana kila mara katika mambo ya msingi na yasiyo na msingi. Kugombana si kubaya kama kunaleta tija, lakini kule kugombana kunakofanywa kwa misingi ya kujitafutia umaarufu kunasabaisha viongozi kushindwa kutekeleza majukumu yao ambayo yanatokana na ahadi wakati wakiomba ridhaa ya kuchaguliwa na wananchi, ni dhambi ambayo haiwezi kuvumilika hata kidogo. 

Wakati tunaelekea katika kipindi cha mchakato wa kupata wagombea wa nafasi ya uraisi kupitia vyama mbalimbali; sisi kama wananchi tuanze kujipima na kujua ni kiongozi wa namna gani tuna mwitaji; tuziangalie khali zetu za uduni wa maisha  sisi bado ni masikini, tunahitaji barabara bora; huduma za afya nzuri, elimu bora kwa vijana wetu; ajira za kutosha kwa wenye sifa za kuajiriwa; 
 


Kama Rais Kenedy wa Marekani alivyowahi kusema ‘Wewe UMELIFANYIA NINI TAIFA LA TANZANIA’ ni wajibu wa msingi kwetu kama wapiga kura kujiuliza swali hili je tumelitendea haki Taifa kwa kuchagua kiongozi bora kwa ajili ya serikali zetu mbili? Yatupasa kutimize wajibu wetu kwa maisha bora kwa kila mtu kwa kuchagua viongozi bora na sio bora kiongozi. Miaka mitano ni mingi sana tukichagua kiongozi mbovu.

Wananchi tujiulize je kama taifa  tumaini letu ni lipi dhidi ya viongozi wetu wa siasa ambao tunatarajia kuwachagua; tunahitaji viongozi wakuu wa nchi ambao wataweza  kutupeleka kwenye nchi yenye neema na amani kwa watu wote bila kujali itikadi, hali yao kiuchumi, kisasa, kidini .

Niliwahi andika huko nyuma kuwa wanasiasasa tukiwaendekeza sana wanaweza kutufanya tusiendelee;tukumbuke kuwa maendeleo yetu kwanza yatatokana na sisi wenyewe, juhudi zetu na misimamo yetu;  tukiangalia kwa ujumla wanasiasa  wanpoteza muda mwingi katika propaganda na sio kutuelimisha ili tuweze kujua kwa undani matatizo na mahitaji yetu yanatokana na nini na tutaweza vipi kuyaondoa.

Wanasiasa wetu ndio wapiga majungu namba moja; aaa siasa zetu zimejaa majungu, chuki tusipoangalia sisi wananchi tutaendelea kuwa wajinga; tusifanye ujinga kuwa ni sehemu ya utamaduni wa siasa za Tanzania kwa kuwachagua viongozi watakao endeleza umasikini wa Taifa letu kwa faida ya wachache.

Kiongozi tunaemtaka tunataka asimamie maono ya kule tunakotaka kwenda na hata kama ana maono yake basi kwa kipindi tunachompa dhamana awe na uwezo wa kuweka misingi ya kufuatilia maono ya kule tunakotaka kwenda sisi kama Taifa.

Je kiongozi tutakaye mchagua atakuwa na mbinu gani za Kujenga uchumi wa ndani, kukuza kipato cha watu wa hali ya chini na kuhakikisha huduma zote muhimu zinamfikia kila mtu hasa wale wananchi wa vijijini ambao ndio wapiga kura namba moja?


Taifa letu katika kipindi cha miaka ya karibuni kiliingia katika vurugu za Mtwara, Dar es salaam Zanzibar Arusha Mbeya Mwanza na kadhalika; Je kiini cha vurugu hizi kimepata jibu? Kama jibu ni hapana sasa tutahitaji viongozi wetu wakuu tutakao wachagua wawe wanaweza kuona na kutumia muda wao katika kuleta majibu ya matatizo ya wananchi wao;
 


Wananchi tunatakiwa tuamke na tusiwape nafasi wanasiasa kutufanya sisi kuwa  daraja lao la wao kuweza kutimiza malengo yao bila sisi kujitambua kwa haraka; matokeo yake ni sisi ambao ndio tunapigwa, tunauwawa na tunaendelea kuwa masikini.

Imefika wakati sasa hata viongozi wengine tutakao wachagua tusirudie kosa la kuchagua viongozi ambao wanasilka na tabia ya
kuzomeana, kulaumiana, kutukanana;mwelekeo huu hautatusaidia sisi lengo letu la kuwa na maisha bora

Nafikiri linalowezekana leo lifanyike leo kwani hakuna kesho katika maendeleo ya binadamu kwani sisi tunaishi leo na sio kesho; kesho inabaki katika hazina ya Muumba wetu tu;

Baba wa Taifa aliwahi kusema kuwa “Kupanga ni kuchagua”. Wananchi kwa kweli inatakiwa tujipange sasa kwa maendeleo ya Taifa letu na kwa masilahi yetu binafsi ili kupata viongozi wetu wakuu walio bora na makini. Tunataka tupate viongozi waadilifu kweli kweli.

Tukumbuke kuwa Uadilifu ni karama, ya utambuzi wa kujifahamu kwa mtu binafsi hususa kiongozi wa serikali, ambaye anatakiwa kufanya kazi zake kulingana na sheria na taratibu ambazo hujenga, utamaduni, wa kuwajibika kulingana na  sheria husika. Kwa kufuata taratibu nzuri za utendaji kazi  Uadilifu katika kazi husaidia uimarishaji wa misingi ya utawala bora.
 


Kwa kujumuisha kabisa uadilifu na utimilifu kwa uhusiano wa biashara yetu inayoendelea na kufanya uamuzi, tunaonyesha kujitolea kwa utamaduni ambao unakuza kiwango cha uadilifu wa hali ya juu kabisa; ni kweli kuwa uadilifu inahitaji uaminifu binafsi wa kiongozi husika; uadilifu unahitaji  uaminifu wa kupinga ubinafsi kwa kiongozi ambaye amepewa dhamana. Uadilifu unaendana na Kuwa mkweli katika utendaji na kuishi kulingana na maadili ya kazi na kuheshimu rasilimali kwa faida ya wengine.

Wajibu wa kutenda ukweli ni wajibu wa juu kabisa wa uadilifu kwa viongozi wa umma; kiongozi wa umma lazima  atambue hali halisi ambayo inaendana na wajibu kwa kufuata maadili hivyo kusambaza cheche ili hata jamii nzima nayo iweze kuishi kulingana na maadili ya Taifa.

Kiongozi mwadilifu daima hutakiwa kuonyesha uhusiano kati ya maadili yake ya utendaji na kwa urahisi kabisa aweze kusema na nafsi yake ili  isitawaliwe na tama ya rushwa ambayo itapingana na dhana nzima ya maadili kulingana na kiapo chake. Hapa ni jukumu la serikali kuweka mipaka bayana wa uhusiano kati ya maadili binafsi na sheria za utendaji wake kwa manufaa ya umma. Uadilifu daiama huashiria haki, ikiwa na maana kuwa kiongozi wa umma lazima aweka maslahi binafsi pembeni;

Uadilifu hujenga amani, huleta ufanisi, kwani Watumishi wa umma watakuwa wanauwezo wa kuhakikisha matumizi sahihi, ufanisi wapesa za umma. dhana na misingi ya uwajibikaji anatarajiwa kufanya ya viongozi wa umma kuwajibika kwa matendo yao au kutotenda

Ni zinatakiwa kuongeza uwazi wa serikali, kusisitiza na kuimarisha mwitikio wa kiserikali na uhalali na kuboresha utekelezaji wa sera. Mwalimu Nyerere katika hija ya maisha yake, alijitahidi kutanguliza masilhai ya watu wake, bila ya kujikita katika ubinafsi, uroho na uchu wa madaraka; uchoyo na ubinafsi; dhambi zinazoendelea kuwatesa viongozi wengi ndani ya Taifa letu.
 


Maadili ni muhimu zaidi na katika siasa na kwa maendeleo ya wananchi. Maadili ya kweli yatapunguza wanasiasa kujishughulisha na rushwa. 

MUNGU IBARIKI JAMUHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA NA UTUVUSHE SALAMA ILI TUWEZE KUWAPATA VIONGOZI BORA KWA MANUFAA YA WATU WAKO katika uchaguzi wa mwaka huu 2015.