WHATEVER YOUR ARE BE A GOOD ONE;

A nation that is afraid to let its people judge the truth and falsehood in an open market is a nation that is afraid of its people. John F. Kennedy

“Taifa letu – taifa lolote – ni zuri na mahali pazuri pa kuishi kama raia wake watalifanya liwe hivyo. Uongozi wake unaweza kuwa mzuri, mbaya au usiojali lakini kama watu wake wameamka (ki-elimu?) na wanajitambua, haitachukua muda mrefu kuwakilisha mtazamo wa jamii na kubadili mawazo na matumaini ya taifa.” Julius Kambarage Nyerere


Friday, August 15, 2014

Si kila kiongozi ana akili ya kuongoza


Uongozi hauji na akili MOJA ya tunu kubwa ambayo Mwalimu Julius Nyerere alituachia kama taifa ni kuwaamini sana viongozi. Mwalimu tulimpenda na tulimwamini karibu kwa kila jambo alilosema na kutenda. Kilichofanya Watanzania tumwamini sana mwalimu sio kwamba alikuwa ni malaika.

 Mwalimu Nyerere aliaminika kwa sababu tatu kubwa kwa maoni yangu, ambazo ni ukweli, uhalisia na kujua mambo. Mwalimu kama kiongozi alikuwa ni mkweli, mhalisia na alijua kikamilifu alichokisema na kukitenda. Hizi ni bidhaa adimu kabisa katika uongozi uliofuata baada ya Mwalimu.

 Kwa kuwa tulimwamini sana Mwalimu Nyerere, na kwa kuwa alikuwa anajua mambo mengi na kwa upana wake, tulimsikiliza sana na kukubaliana na karibu kila kitu alichokizungumza na kukifanya. Hata pale tulipojua Mwalimu alikosea hatukumsuta kwa sababu tulijua hakukosea kwa kutaka au kwa makusudi. Tulimpa kile wazungu wanakiita ‘benefit of doubt’ kwa sababu ya ukweli na uhalisia uliokuwa dhahiri. Kwa imani yetu kwa Mwalimu ilifika mahala kama vile ‘tukajiuzulu’ kufikiri, kwa sababu tulikuwa na mtu anayefikiri kwa niaba yetu.

 Kwa hiyo nchi ikiwa katika msukosuko, tulisubiri kusikia Mwalimu anasemaje katika hili. Ndivyo ilivyotokea kwa vita ya Kagera. Kabla ya Mwalimu hajazungumza, taifa lilikuwa limezizima tusijue cha kufanya, lakini alipozungumza wote tulikubaliana naye. Ndivyo vile vile ilivyotokea wakati taifa lilikuwa kama halijui likubali mfumo wa vyama vingi au la. Viongozi wengi wa CCM walikuwa wamepinga vikali kuanzishwa kwa mfumo wa vyama vingi, lakini mara baada ya hotuba ya Mwalimu kwa vijana huko Mwanza, wote tukageuka na kukubaliana na mfumo wa vyama vingi.

 Kwa hiyo Mwalimu alipandikiza mbegu ya uaminifu kwa viongozi. Tumeendelea kuwaamini viongozi hata baada ya Mwalimu kuondoka madarakani na duniani. Tumeendelea kuwaamini kwamba tuna viongozi wanaofikiri kwa niaba yetu na sisi hatuna sababu ya kuhangaisha bongo zetu zaidi ya kuchangamkia matamasha ya Fiesta ambayo nayo yanafunguliwa na viongozi wetu huko mikoani.

Tunadhani kwamba mtu akishapewa uongozi anapewa na akili! Kwa hiyo hatuwapimi viongozi wetu kwa uwezo na historia yao kabla na baada ya kupewa uongozi, bali kwa sababu ni viongozi wanajua na wanaaminika, kwa sababu moja tu - ni viongozi. Sisi tunaendelea kuamini kwamba kila aliye kiongozi ana akili za kuongoza! Ambacho hatujang’amua ni kwamba yale ambayo yalitufanya tumwamini Nyerere ni mambo adimu sana katika uongozi wa leo. Utakuwa na bahati kubwa ukikutana na kiongozi aliye mkweli, mhalisia na anayejua mambo katika nchi hii. Na hapa sizungumzii tu uongozi serikalini; ni kote –katika serikali, mashirika ya umma, vyama vya siasa na maeneo mengine mengi.

Viongozi wetu wengi wana akili za kuagizwa. Ukimuuliza kwa nini unafanya jambo hili la ovyo kabisa, jibu lake ni kwamba wakubwa wameamua. Mkubwa naye ukimuuliza anakwambia hivyo hivyo, kwamba wakubwa wameamua. Yote hii ni kwa sababu si wa kweli, si wahalisia na wala hawajui sawa sawa mambo wanayoyasimamia. Na hawajui kwa sababu hawajishughulishi kujua wakiamini kwamba kwa kuwa wao ni viongozi wanajua!

Ni kwa sababu ya kuwaamini sana viongozi wasio wa kweli, wasio na uhalisia na ambao hawajishughulishi kujua mambo tumeanza kushuhudia mambo ya ajabu katika nchi hii. Tumefika mahala watu wanauawa mbele ya viongozi kama ilivyotokea huko Iringa. Lakini kwa sababu ya kutokuwa wa kweli na kukosa uhalisia, viongozi wetu wanajaribu kusema uongo bila aibu kwamba kilichomuua marehemu ni kitu kizito kilichorushwa kutoka kwa raia. Kiongozi huyu anafanya hivyo kwa sababu anajua kwamba ataaminiwa kwa sababu Watanzania walipandikiziwa mbegu ya kuamini viongozi siku nyingi.

Kiongozi mwingine naye anakurupuka bila aibu na kutangaza kwamba nitakifuta chama fulani kwa sababu kinasababisha vurugu katika nchi. Kiongozi anajua anadanganya kwa sababu anajua fika kwamba vurugu zinasababishwa na vyombo vilivyopewa jukumu la kuzuia vurugu. Lakini kiongozi huyu anapata ujasiri wa kusema uongo kwa sababu si mkweli wala mhalisia, lakini muhimu zaidi ni kwa sababu anajua kwamba Watanzania watamwamini kwa sababu ni kiongozi.

 Utamaduni wetu wa kuwaamini sana viongozi ndio uliosababisha mashirika ya umma kufa kwa sababu viongozi walikuwa wanafanya mambo ya kipuuzi huku wafanyakazi wakiwaangalia kwa sababu ni viongozi. Na sasa wafanyakazi wa mashirika ya umma wanaendelea kushuhudia mashirika yakifa kwa sababu ya imani waliyonayo kwa viongozi wao wanaofanya upuuzi. Vinginevyo, tutaelezaje kitendo cha mashirika kama ATC, Bandari na TANESCO kufika hapo yalipofika huku wafanyakazi (wazalendo?) wakiwapo? Ni kipi kilichowafanya wafanyakazi wa mashirika haya kuvumilia upuuzi uliokuwa ukifanywa na viongozi hadi mawaziri walipoingilia kati kwa sababu za kisiasa?

 Hatua muhimu ya kuwafanya viongozi wetu kuamka ni kupunguza imani yetu kwao. Tukipunguza imani yetu kwao watafanya bidii ili waweze kuaminika. Na ili waweze kuaminika itabidi wajifunze ili kupanua uwezo wao wa kiakili na kiutendaji. Tatizo tulilonalo sasa ni kwamba viongozi wetu wengi hawana bidii ya kujifunza. Ni wachache wanaosoma vitabu. Hawaandiki, na kwa hivyo hatujui wanachokifikiria. Kibaya zaidi, hata mambo madogo kama kuhudhuria makongamano na mijadala mbalimbali hawapo, na hasa makongamano yasiyo na posho. Kwa hivyo, sisi kama wananchi hatuna njia ya kujua viongozi wetu wanafikiri nini na wanajua nini. Tumeendelea kuwaamini kwamba kwa sababu ya imani yetu ya muda mrefu kwamba viongozi wanajua.

Ukweli ni kwamba uongozi haumpi mtu akili, bali unaweza kumpatia fursa ya kujifunza kama anataka kujifunza. Ndio kusema kama mtu ni mjinga leo, ataendelea kuwa mjinga hata kama atapewa nafasi ya uongozi kesho kama hatafanya bidii ya kujielimisha. Uongozi hauondoi ujinga. Kwa hiyo tuache kuamini kila jambo linalosemwa na viongozi kwa sababu tu ni viongozi. Hii ni muhimu zaidi katika kipindi hiki ambacho taifa lina uhaba mkubwa wa ukweli na uhalisia miongoni mwa viongozi wa kizazi cha leo. Kwa maneno mengine, hakuna Nyerere wa kufikiri kwa niaba yetu na ni lazima sasa tuanze kujitegemea katika kufikiri. -

No comments:

Post a Comment