WHATEVER YOUR ARE BE A GOOD ONE;

A nation that is afraid to let its people judge the truth and falsehood in an open market is a nation that is afraid of its people. John F. Kennedy

“Taifa letu – taifa lolote – ni zuri na mahali pazuri pa kuishi kama raia wake watalifanya liwe hivyo. Uongozi wake unaweza kuwa mzuri, mbaya au usiojali lakini kama watu wake wameamka (ki-elimu?) na wanajitambua, haitachukua muda mrefu kuwakilisha mtazamo wa jamii na kubadili mawazo na matumaini ya taifa.” Julius Kambarage Nyerere


Friday, November 9, 2012

Toto waahidiwa sh 500,000 kila mmoja wakiifunga Simba




WACHEZAJI wa Toto African wameahidiwa ya sh 500,000 kila mmoja endapo watafanikiwa kuifunga Simba kesho katika mchezo wao wa mwisho wa mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu utakaopigwa kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Pamoja na ahadi hiyo nzuri kutoka kwa viongozi wao bado wachezaji wa klabu hiyo wanashangaa ni wapi uongozi wao umepata fedha hizo za kuwapa motisha wakati hawajawalipa mishahara yao ya miezi minne iliyopita.

Wakizungumza na Mwananchi jana kwa sharti la kutotajwa majina yao baadhi ya wachezaji hao walisema kuwa hivi karibuni viongozi wa timu hiyo waliwataka kuhakikisha wanaifunga Simba na wakifanikiwa kila mmoja ataondoka na sh 500,000 ikiwa ni pamoja na kulipwa madai yao yote wanayodai.


"Motisha hiyo imeongeza morali katika kambi yetu na kila mchezaji amepania kuhakikisha hatupotezi mechi hiyo angalau tuweze kuishi maisha mazuri kidogo wakati ligi itakapokuwa imesimama,"alisema mmoja wa wachezaji hao.

"Tunashangaa ni wapi viongozi wetu wamepata fedha hizo sababu hadi sasa tulikuwa bado hatujalipwa mishahara yetu ya miezi minne iliyopita," alisema mchezaji mwingine.

Habari za uhakika kutoka ndani ya klabu hiyo zinadai kuwa viongozi wa Toto wamepokea fungu la kutosha kutoka kwa klabu za Yanga na Azam ili kuhakikisha Simba inaendelea kubaki katika nafasi ya tatu.

Jana asubuhi mara baada ya mazoezi ya Toto baadhi ya viongozi wa timu hiyo walionekana wakiwa na viongozi wa Yanga.

Msimu uliopita Simba ililazimishwa sare 0-0 na Toto African kwenye mchezo uliofanyika Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Katika hatua nyingine msemaji wa Simba, Ezekiel Kamwaga amelalamikia kitendo cha Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kurudisha nyuma mchezo wao tofauti na wapinzani wao wa jadi Yanga.

Kamwaga amelalamikia kitendo hicho kwa madai kuwa kinaashiria kuibeba Yanga na kuna uwezekano mkubwa wa kuhujumiwa na wapinzani wao kutokana na upinzani mkubwa uliopo kati yao katika mbio za kuwania ubingwa msimu huu.

TFF juzi ilitangaza kuzirudisha nyuma kwa siku moja mechi zote za mwisho za mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu, kutoka Jumapili wiki hii hadi Jumamosi, isipokuwa mechi ya Yanga na Coastal Union imebaki siku ya Jumapili itakayochezwa Uwanja wa Mkwakwani, Tanga.

Akizungumzia kwa nini mechi ya Yanga na Coastal Union haijarudishwa nyuma Katibu wa TFF, Angetile Osiah alisema,"sababu ya kutorudishwa nyuma mechi ya Yanga ni kwa kuwa siku ya Jumamosi kutakuwa na mchezo mwingine wa ligi hiyo kwenye  Uwanja wa Mkwakwani kati ya Mgambo JKT na Azam FC."

Kulingana na mabadiliko hayo, Simba sasa itamaliza mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu siku ya Jumamosi Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam dhidi ya Toto Africans, wakati Yanga itamaliza na Coastal Mkwakwani siku ya Jumapili.  
 
Mechi nyingine za Jumamosi ni African Lyon na Mtibwa Sugar, Prisons na JKT Ruvu, huku Kagera Sugar ikicheza na Polisi Morogoro wakati JKT Oljoro watakipiga na Ruvu Shooting.

source; Vijimambo.blog

No comments:

Post a Comment